Muswada wa Bima ya Haufai. Utupiliwe Mbali

OFISI YA WASEMAJI WA KISEKTA.

HIFADHI YA JAMII NDIYO MWARUBAINI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE; MUSWADA WA BIMA YA AFYA NI WA KUTUPILIWA MBALI!
Ndugu Waandishi wa Habari,


A. Utangulizi:
Muswada wa sheria ya ‘Bima ya Afya Kwa Wote’ uliwasilishwa Bungeni rasmi tarehe 23 Septemba 2022 na unatarajiwa kuanza kujadiliwa katika ngazi ya Kamati ya Bunge kesho Jumatatu tarehe 10. Mswada huu umeleta hisia mchanganyiko miongoni mwa Wadau, Wananchi na Wanasiasa na kwa pamoja, jambo tunalokubaliana ni kwamba Muswada wa Bima ya Afya umekuja katika kipindi ambacho kumejitokeza dalili za wazi za kutokuwa na usawa wa upatikanaji wa huduma bora za afya.
Mwanya huu wa usawa unaonekana kati ya Wananchi walioko mijini na vijijini kwa upande mmoja; na walala hoi mijini na watu wenye nacho (matajiri) kwa upande mwingine. Wakati Wananchi vijijini wamekuwa wakipata huduma duni za afya, vivyo hivyo walalahoi na wavujajasho wa miji wanashindwa kumudu gharama za matibabu na huduma nyingine za afya. Wengi wetu ni washuhuda wa ndugu na jamaa zetu wanaotaabika n ahata kupoteza maisha kwa kushindwa kugharamia matibabu yao. Taifa letu limefika mahala hata ndugu hugomewa kuchukua maiti za wapendwa wetu kwa sababu tu ya kushindwa kumudu gharama. Pamoja na hali hii, inaumiza na kusikitisha kwamba kuna kundi dogo la Wananchi wanaofurahia huduma zenye uhakika za afya.

Tumefikaje Hapa?
Kukosekana kwa usawa katika kugharamia huduma za afya kumesababishwa na Serikali kujitoa kwenye Wajibu wake wa kugharamia huduma za afya. Serikali imetengeneza mfumo ambao, asilimia 100 ya gharama za afya ni mzigo wa Watanzania – jambo ambalo ni la aibu kwa taifa letu. Takwimu zinaonyesha, idadi ya Wananchi kuugua inazidi kuongezeka kila uchao. Kwa mujibu wa Taarifa za Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2021; zinaonyesha jumla ya watu milioni 41 ambao ni 70% ya Watanzania wote waliugua na kwenda kwenye vituo vya huduma ya afya kama wagonjwa wa nje.
Kwa kuzingatia idadi kubwa ya Wananchi wanaougua nchini, Serikali makini ilipaswa kulipa suala la afya ya jamii uzito na kipaumbele cha kipekee, kwa kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora kwa usawa na haki.
Matarajio ya wengi ni kwamba; Muswada mpya wa Afya ungeenda kutatua kiini cha kukosekana kwa huduma bora ya afya kwa Wananchi wote mijini na vijijini LAKINI, hii ni tofauti na matarajio.
Mfumo bora wa Afya unategemea kuwepo kwa nguzo kuu saba ambazo ni utawala bora, mfumo bora wa ugharamiaji, uwepo wa dawa na vifaa tiba, wafanyakazi wa afya, ukusanyaji na utumiaji wa takwimu za afya, ushirikishwaji wa jamii na uwepo wa vituo vya kutolea huduma za afya. Ni Dhahiri kwamba Serikali imekuwa ikipuuza nguzo hivi na ndiyo maana Taifa limefika hapa tulipo. Ili tupate mfumo imara kuna umuhimu mkubwa wa kuimarisha nguzo hizi ili kupata mfumo bora wa afya nchini.
ACT Wazalendo katika kutimiza Wajibu wetu wa kutetea maslahi ya Watanzania wote na kuhakikisha Serikali inafanya hivyo pia; kupitia Wasemaji wa Sekta ya Afya na Sekta ya Uwekezaji na Mashirika ya Umma tumeutazama kwa makini Muswada huu, tumeuchambua na kuja na mapendekezo ambayo yatahakikisha huduma ya afya inaboreshwa kwa maslahi ya Watanzania wote na siyo tuu, kunufaisha watu wachache.

B. Mapungufu Tuliyoyabaini kwenye Muswada wa Afya:
Mosi, Muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote hauendi kubadili Mfumo uliopo hivi sasa wa ugharamiaji wa huduma za afya ambao umeachwa kwenye mabega ya Mwananchi kwa asilimia 100 aidha kwa kutumia pesa taslimu au kwa kupitia mfumo wa Bima ya Afya.
Pili, Mswada huu unalenga kuongeza idadi ya wanachama wa mfuko wa Bima ya Afya kwa Umma kabla ya kutatua matatizo yaliyokwamisha ufanisi wa NHIF. Mfuko wa Bima ya Afya kwa Umma unarithi matatizo ya upotevu wa fedha yaliyoelemea NHIF. Ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonyesha kuna malimbikizo ya makusanyo yanayofikia shilingi bilioni 8.7 kutoka kwa taasisi za umma na wizara, pia kuna upotevu wa fedha unaotokana mikopo ya shilingi bilioni 98.5 iliyoiva iliyotolewa kwa taasisi za Serikali ambayo haijalipwa, na mkopo wa shilingi bilioni 129 uliotolewa kwa Serikali bila mkataba, mkopo huu pia bado haujalipwa. Zaidi ya hayo kuna uwekezaji mkubwa kwenye kiwanda cha bidhaa za tiba cha Simiyu ambao bado haujazaa faida. Hatuwezi kuendelea kuifumbia macho Serikali ikifanya mambo kama haya.
Tatu, muswada umeeleza adhabu zitakazotolewa kwa watumiaji na watoa huduma watakao kiuka sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, lakini haijaelezea udhibiti wa ubadhirifu wa fedha za Mfuko wa Bima kupitia mamlaka za Serikali. Aidha, muswada umeipa Serikali kupitia kwa Waziri mwenye dhamana mamlaka yatakayoingilia majukumu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima. Hivyo, muswada huu unachochea muendelezo wa ubadhilifu wa fedha za mifuko ya hifadhi za jamii ulioanza miaka ya nyuma.
Nne, Mswada umeeleza kufutwa kwa Mfuko wa Afya ya Jamii (Community Healthy Fund) na kuwalazamisha Wananchi wenye kipato kidogo kuingia kwenye Skimu ya Bima ya Afya kwa Umma, skimu inayorithi vifurushi vya NHIF ambavyo ni vya gharama kubwa na mapungufu kama kutolipia huduma kwa magonjwa ya saratani, figo na moyo, huduma za kliniki za wajawazito na kuondoa huduma muhimu za rufaa kwa watu wenye kipato kidogo. Hivyo, mswada huu unaimarisha mfumo mbovu unaoendelea wa utoaji wa huduma ya afya nchini, mfumo unao weka na kuimarisha matabaka kwenye jamii kwa kuifanya huduma ya afya iwe bidhaa, na kuongeza ugumu wa hali ya uchumi kwa Mwananchi.
Tano, muswada umeweka vigezo vya kupata leseni, Pasi ya kusafiria, Kitambulisho cha NIDA, laini za simu hadi uwe na kadi ya Bima ya Afya. Tukijiuliza ni kama vile Serikali haijajipanga vizuri; hivi haki ya NIDA na Bima kipi kinaanza?
Utaratibu huu unawanyima wananchi uhuru na haki yao ya msingi ya kupata huduma hizo ambazo tayari wanazilipia kupitia kodi na tozo mbali mbali. Serikali haijajiandaa, sheria hii haitekelezeki, nikupoteza muda tuu. Serikali irudi tena mezani, Sisi ACT Wazalendo tuko tayari kushirikiana nao ili kuja na mpango bora wa kupata Bima ya Afya kwa Wananchi wote.
Sita, Utambuzi wa watu wasio na uwezo: katika maelezo yake Waziri wa Afya ameeleza kwamba watu wasio na uwezo watatambuliwa kupitia taarifa za unachama wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). Takwimu za Hali ya Uchumi wa Taifa mwaka 2021 zinaonyesha jumla ya watu milioni 6.3 sawa na 11% ya wananchi wote walinufaika na mfuko wa TASAF. Idadi hii ni ndogo kulinganisha na hali yalisi ya umaskini nchini ambapo idadi ya watu wanaoishi chini ya mstari wa umaskini wa mahitaji ya msingi ya dola moja kwa siku ni karibia asilimia 26.4 ya wananchi wote. Utaratibu huu hautajumuisha watu wengi zaidi wenye kipato kidogo kwenye sekta isiyo rasmi wasio na vigezo vya kunufaika na TASAF.
Mwisho, Muswada huu haujagusa kichocheo cha ongezeko la gharama za dawa, vifaa tiba na vipimo ambao unaamuliwa na soko la dawa.


Kwahiyo, Mswada huu ukipitishwa utakuwa sheria itayogeuza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuwa Skimu ya Bima ya Afya kwa Umma, inafuta Mfuko wa Afya ya jamii (Community health Fund) na kuwalazimisha wananchi wote kuwa na bima ya afya.

C. Mapendekezo ya ACT Wazalendo:
1. Kila Mwananchi mwenye ajira Rasmi na kukatwa michango ya Hifadhi ya Jamii apate Fao la Matibabu. Mfuko wa NSSF au PSSSF ambao mwajiriwa ana mchango wake utapeleka 1/5 ya mchango wa mwajiriwa kwa Skimu ya Bima ya Afya.

2. Kila Mwananchi aliyejiajiri kwenye sekta ya Kilimo, Biashara au shughuli nyingine yeyote na ni mwanachama wa hiari katika mfuko wa Hifadhi ya Jamii anayechangia kiwango cha chini cha mchango wa Mwezi (kwa sasa ni Shs 30,000) atachangiwa na Serikali theluthi ya mchango kila mwezi, hii itakuwa kivutio kwa watu walio kwenye sekta isiyo rasmi kujiunga kwenye mfuko wa Hifadhi ya Jamii na kupata Bima ya Afya. Mfuko wa NSSF utawasilisha kwa Skimu ya Bima ya Afya 1/5 ya mchango huu kila Mwezi kwa ajili ya Fao la Matibabu la mwanachama. Tofauti na sasa mwanachama atatakiwa kuchangia 340,000 kwa mwaka kwenye Mfuko wa afya kwa ajili ya matibabu pekee.

Kwa hiyo kila mwenye kadi ya NSSF/PSSSF moja kwa moja anakuwa ana kadi ya Skimu ya Bima ya Afya. Bima ya Afya inakuwa ni fao tu Katika moja ya mafao ya Hifadhi ya Jamii lakini uendeshaji wake unafanywa na Skimu ya Bima ya Afya.

3. Mtu yeyote ambaye ni mnufaika wa TASAF atalipiwa mchango wake na Serikali moja kwa moja kwenye Hifadhi ya Jamii kwa 100%. Hata hivyo mfuko wa Hifadhi ya Jamii utakuwa na Fao Maalumu la kuwawezesha kuzalisha kipato ili kufikia kundi la kuchangiwa theluthi tu.

4. Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) isimamie na kudhibiti Skimu ya Bima ya Afya badala ya Mamlaka ya usimamizi wa Bima (TIRA) kama ilivyo sasa.
Kwa mapendekezo haya ya ACT Wazalendo, tuna uhakika wa kila Mtanzania mwenye umri zaidi ya miaka 18 kuwa na Bima ya Afya kama fao miongoni mwa mafao ya Mfumo wa Hifadhi ya Jamii nchini. Taarifa za hivi karibuni zinaonyesha idadi ndogo ya wanufaika wa Bima za afya na Mfuko wa Hifadhi ya jamii. Jumla ya watu milioni 17 sawa na karibia 33% ya watanzania wana nufaika na Bima za afya za NHIF na CHF, na jumla ya watu milioni 1.6 sawa na 2.7% wamejiunga na PSSSF au NSSF.

D. Fedha za Serikali kuchangia zitatoka wapi?

1. Serikali itenge kila mwaka katika bajeti yake 2.5% ya Pato la Taifa la Mwaka uliotangulia kama fedha za kuchangia mfumo huu. Kwa thamani ya sasa ya pato la taifa hii ni sawa na Shs 3.5 trillioni.

2. Serikali haitakuwa tena na jukumu la kuendesha vituo vya kutoa Huduma za Afya kwani kwa mfumo huu vituo vitajiendesha vyenyewe na kwa ufanisi mkubwa.

3. Uwezo wa nchi kuweka akiba utakuwa mkubwa na hivyo Serikali kuwa na fursa ya kupata Fedha za ndani kuwekeza kwenyemiradi ya kimkakati itakayowezesha watu wengi zaidi kuwa kwenye ajira rasmi na hivyo kupunguza Kundi kubwa la kuchangiwa.

Hitimisho
Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inapeleka Bungeni Muswada wa kuwalazimisha watu kwa nguvu kuwa na Bima ya Afya. ACT Wazalendo, tunaitaka Serikali iachane na mpango huo na itupilie mbali muswada huu na irudi upya mezani kutengeneza mfumo unaomjali Mtanzania wa kila hali. Tunasisitiza wito wetu wa kutazama upya Mfumo wa Hifadhi ya jamii (Social Security System) ili ndani yake uwe na Bima ya Afya inayowezesha utoaji wa huduma bora za Afya kwa Watanzania wote na kwa haki na usawa bila kuathiri zaidi hali ya uchumi ya Mwananchi mmoja mmoja. Mpango huu tunaoupendekeza utawavutia (incentivise) wananchi kuwa na Bima ya Afya.
Imetolewa na:


Ndg. Ruqayya M. Nassir
Naibu Msemaji wa Sekta ya Afya
Twitter:


Ndg. Mwanaisha Mndeme
Msemaji wa Sekta ya Uwekezaji, Mashirika ya Umma na Hifadhi ya Jamii
Twitter:

 

 

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK