Semu: Wanawake ni Jeshi la Ukombozi. Tuunganishe nguvu zetu

SEHEMU YA HOTUBA YA NDG DOROTHY SEMU KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI TAREHE 8 MACHI, 2022 MKURANGA-PWANI

*Wanawake ni jeshi la Ukombozi: Siku ya Leo Tuunganishe nguvu zetu.*

Ninajisikia furaha sana kuwa sehemu ya watu ambao leo kwa umoja wetu ni siku muhimu katika kuamua na kujenga mustakabali bora wa jamii yetu.

Pili, nikiwa kama sehemu ya jamii ambayo imenipa wajibu mkubwa wa kiuongozi katika kuhakikisha watu wanafikia ndoto zao za kuwa kwenye jamii yenye furaha, isiyokuwa na unyanyasaji, ukandamizaji na udhalimu, ninajiona mtu mwenye deni mbele yenu na watanzania wengine.

Siku hii ni muhimu sana kwetu (Wanawake) kutokana na ukweli kwamba inatupatia wasaha wa kuimulika nchi na kuona nafasi ya wanawake katika pembe mbalimbali ikiwemo uongozi, uwakilishi, hali ya kimaisha na upatikanaji wa fursa.

Ninaamini kuwa kwetu sio mara ya kwanza kuadhimisha siku hii au kuona makundi mbalimbali ya kijamii yakiadhimisha kwa mitindo na programu zinazoakisi tafsiri waliyonayo kuhusu siku hii adhimu. Hivyo awali kabisa ningependa nichagize tu kuiadhimisha kipekee kabisa ambayo itatoa uelekeo wa Chama chetu na uelewa mzuri kuhusu siku ya Wanawake duniani. Na kuadhimisha kipekee kutawezekana ikiwa tutaelewa msingi na historia halisi ya siku yenyewe ambayo itatuonyesha tulikotoka na kutusaidia kujua tulipo na kisha kuona namna mustakabali wetu tunaoutaka.

Miaka takribani mia mbili iliyopita, wanawake wenzetu walifanya uamuzi wa kukataa ubaguzi uliokuwepo katika siasa na jamii. Katika siasa wanawake wa wakati huo hawakuhesabika kama watu wanaoweza kupiga kura sio tu kuchagua lakini hata kuchaguliwa. Hivyo hawakuwemo kwenye vyombo vya uamuzi au hawakuweza kuamua nani wamchague.

Pia, katika ajira walikuwa wanalipwa ujira kiduchu sana tofauti na wanaume, hawakuwa na likizo ya uzazi, masaa ya kazi yalikuwa hadi 14 kwa siku, kwa kifupi mazingira ya kazi hayakuwa rafiki.

Hivyo, Wanawake wavujajasho katika viwanda waliamua kukataa udhalimu huo kwa maandamano na migomo. Walisaidia kuleta mabadiliko muhimu tunayoyaona leo ambayo yaliwanufaisha hata wafanyakazi wanaume. Jitihada zao hazikuishia hapo tu, tungeweza kuorodhesha kwa urefu sana. Lakini itoshe kwa mifano hiyo michache.

Mavuguvugu ya madai mbalimbali ya wanawake kudai usawa wa kijinsia yamechukua sura tofauti tofauti kutokana na nyakati mbalimbali hadi sisi tunayakuta. Basi, nasi tunao wajibu wa kuendeleza mapambano hayo. Hatuwezi kushirikiana kuondoa vikwazo, unyanyasaji, ubaguzi na ukandamizaji dhidi yetu kama hatujaangazia hali ilivyo hivi sasa.

*Hali yetu bado sio nzuri*

Kwa miongo takribani miwili, harakati za wanawake zilipamba moto hata kufikia kupata mafanikio kadhaa hususani linapokuja suala la nafasi za uongozi wa kisiasa. Takwimu zinaonyesha tumepiga hatua lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya. Kwa Mfano, wanasiasa viongozi wanawake katika ngazi ya udiwani bado ni takriban asilimia 5 tu. Nchi yetu ina kata takriban 400.

Pamoja na jitihada hizo, bado kuna ukweli unatusakama kuhusu mapambano yetu. Wapo Wanawake wenzetu tumewaacha nyuma ambao ni wengi zaidi. Wanawake ambao hawamo kwenye siasa, asasi za kiraia wala kwenye sekta ya umma. Hawa ni wanawake waliopo kwenye sekta ya ajira isiyo rasmi (ama kwenye kilimo au sekta isiyokuwa ya kilimo) kundi hili ni kubwa, na hata ukubwa wa athari za udhalimu dhidi yao ni mkubwa.

Nyinyi hapa ni mashahidi katika maadhimisho haya mmetembelea hospitali kadhaa tena zilizopo jijini Dar es Salaam. Hali ni mbaya, huduma ni za kusuasua. Kama Dar es Salaam ipo hivi, vipi kuhusu vijijini huko? Nani anayewasikia na kuwajali, pengine hata siku hii kwao kama wangepata nafasi wangeitumia vinginevyo sio kusherehekea, aidha kuomboleza, kunung'unika, kupiga kelele au kuandamana. Hakuna anayejua zaidi yao wenyewe.

Sisi tuliopo kwenye siasa tuhakikishe vyama vyetu vinagusa matarajio, malengo na maslahi yao. Tuungane nao kwa kuwashirikisha, kupaza sauti zao na kusukuma ajenda zao ambazo ni ustawi wa jamii kwa ujumla wake.

Awali nilisema najisikia furaha kujumuika nanyi katika siku ya leo sio tu kwakuwa nimejumuika na Wanawake wenzangu. Ni kwasababu, nimekutana na watu wa chama cha Wazalendo.

Chama chetu, kimekuwa Chama kiongozi katika kupigania usawa wa kijinsia na kuhakikisha maslahi ya wanawake yanazingatiwa. Mambo tunayoweza kutoa mfano wa dhahiri hapa juzi tu tulitangaza kamati ya kuisimamia Serikali (Bunge Kivuli), ambaye Mimi ndio Kiongozi wa hiyo Kamati nikiwa ni Waziri Mkuu Kivuli, pamoja na mimi Wanawake wamechukua asilimia 50 ya wasemaji wa sekta za kuisimamia Serikali ambao ni kumi na mbili (12). Hii ni hatua muhimu sana kiuongozi na kwa mustakabali wetu wanawake.

Sambamba na hilo, Ilani yetu ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 ilikuwa ni Ilani ya kimageuzi linapokuja suala la kuweka mazingira sawa ya kiuongozi na kuondoa vikwazo kwa wanawake katika kushiriki kwenye mchakato wa Maendeleo. Ilani hii ituongoze kwenye madai yetu ya kila siku.

Sitaki niwafariji kwa kuwapa matumaini pekee, hatua zilozochukuliwa na Chama katika kuliendelea lengo la ukombozi wa Wanawake kama nilivyosema awali ni jambo linalotupa nguvu na hamasa kwa kutuhimiza kuwa mapambano yanapaswa kuendelea kwa ushirikiano wetu wote. Lakini jitihada ya chama ni kama 'mto mdogo' katika jamii ambayo imekita mizizi ya kuweka vikwazo vya kufikia lengo letu. Ni wajibu kuubadilisha mto uliotengenezwa na Chama kuwa bahari.

*TUME HURU ni daraja letu la Ukombozi*

Nihitimishe kuwa, hatuwezi kuwa sehemu ya maamuzi ikiwa hatujashiriki kikamilifa katika kuweka mazingira mazuri ya kutufanya tuwe viongozi. Wote ni mashahidi mazingira ya siasa yanapokuwa kandamizi, wanawake tunavuta sana miguu kuingia kwenye michakato ya kiuchaguzi na siasa kwa ujumla. Hivyo kurudisha nyuma shabaha kuu ya ukombozi. Yeyote anayewapenda Wanawake, anapaswa kuunga mkono jitihada za kuondoa vikwazo vya kisiasa, TUME HURU ya uchaguzi ni jawabu.

Nawashukuru sana kwa kuwa pamoja kwenye siku hii muhimu. Sote tutoke na madai ya Tume Huru ya Uchaguzi.

*Ndg. Dorothy Jonas Semu*
*Waziri Mkuu Kivuli_ACT Wazalendo.*
*Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara*
*08 Machi, 2022.*

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK