Taarifa ya Msiba wa Mwenyekiti wa Taifa ACT Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad kwa umma wa Wanachama na Watanzania kwa ujumla:

Leo mnamo saa 6:13 mchana, nimejulishwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwamba Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amefariki dunia. Taarifa rasmi ya Serikali imeshatoka.

Nasikitika kuwataarifu kwamba Kiongozi wetu, Mzee wetu, na Mwamba wa Demokrasia ya Tanzania, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad, amefariki dunia.

Leo asubuhi, majira ya saa 2.00 nilikuwa hospitalini Muhimbili na kuzungumza na jopo la madaktari waliokuwa wanamuhudumia na hali yake ilikuwa inatia matumaini. Hata hivyo mnamo saa 5:26 asubuhi, Mwenyezi Mungu alitwaa roho yake.

Najua kifo cha Maalim Seif kitawashtua na kuwafadhaisha Wanachama wa ACT Wazalendo, Wazanzibari na Watanzania. Maalim Seif amekuwa nguzo muhimu ya ujenzi wa demokrasia ya vyama vingi katika taifa letu na mtetezi mkubwa wa maslahi ya Zanzibar. Kama Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, napenda kuwahakikishia kuwa tutayaenzi maono yake aliyoyaishi wakati wote wa uhai wake.

Nawaomba Wazanzibari na Wanachama wa ACT Wazalendo na Watanzania kwa ujumla wawe na utulivu katika kipindi hiki kigumu.

Taratibu za mazishi ya Kiongozi wetu zitatolewa baada ya mashauriano baina ya Chama, Serikali na familia kwa mujibu wa sheria na taratibu za mazishi ya viongozi.

 

 

 

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto,
Kiongozi wa Chama,
ACT Wazalendo.
17 Februari, 2021.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK