TUNATAKA TUME HURU YA UCHAGUZI KUELEKEA KATIBA MPYA YENYE MAONI YA WANANCHI-Juma Duni

TUNATAKA TUME HURU YA UCHAGUZI KUELEKEA KATIBA MPYA YENYE MAONI YA WANANCHI


(Hotuba ya Mwenyekiti wa Chama Taifa Ndugu Juma Duni Haji kwenye Uzinduzi wa Operesheni Tume Huru ya Uchaguzi, Mrina Hall, Dar es salaam, 20 Machi 2022).

.....

Ndugu Wanachama na viongozi wa Mkoa wa Dar es salaam, kwa vile hii ni mara yangu ya kwanza kufanya mkutano na Wanachama wa Mkoa huu baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama Taifa, naomba nichukue fursa hii adhimu, kwa mara nyingine tena, kuwashukuru Wajumbe wa Mkutano Mkuu Taifa na Chama changu kwa ujumla kwa heshima hii kubwa mliyonipa.

Kama nilivyoahidi mbele ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu, naaomba niendelee kuwahakikishia Wanachama wa Mkoa wa Dar es salaam kuwa nitajitahidi kadri ya uwezo, maarifa na uzoefu wangu wote kuhakikisha kuwa ninatoa mchango wangu kwa kushirikiana na viongozi wenzangu kuhakikisha kuwa Chama hiki kinatimiza malengo yake ya kushika na kuongoza dola.

Leo tumekutana hapa kwa sababu maalum. Nimefarijika kuona mwitikio wa viongozi na Wanachama kutoka kila pembe ya Dar es salaam. Mkoa wa Dar es salaam umepata heshima ya kipekee ya kuzindua Operesheni ya Chama chetu ya Tume Huru ya Uchaguzi Kuelekea Katiba Mpya.

Malengo ya Operesheni hii ni kuhakikisha kuwa tunamfikia kila mwanachama, kiongozi na mwananchi na kuwaelimisha kuwa kwa mazingira yetu ya kisiasa tunapaswa kuipata Tume Huru ya Uchaguzi kuelekea kuipata Katiba Mpya yenye Maoni ya Wananchi.

Ndugu Wanachama,
Sote ni mashahidi wa machungu ambayo tumeyapitia kwenye miaka sita ya Utawala wa Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli.

Ndani ya Nchi yetu, iliyopiganiwa uhuru na Wazee wetu, tuliishi kama yatima au wakimbizi wa kisiasa kwa sababu tu tulikuwa wanachama au viongozi wa vyama vya upinzani. Tulikamatwa, kufungwa, kuteswa, kufilisiwa na kuuawa kwa sababu tu ya kuikataa CCM.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020 umetuachia makovu yasiyo na mfano ambayo hayawezi kufutika kwa urahisi. Wagombea wengi wenye sifa walienguliwa na wale waliopenya katika dirisha la uteuzi, waliporwa ushindi wao. Kwetu Zanzibar, dola halikuona haya kuwatangaza ushindi hata waliopata kura 50 dhidi ya maelfu ya kura za wagombea wetu!!

Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani, Chama chetu kiliyapokea kwa matumaini matamshi ya Mh. Rais Samia Suluhu Hassan kuwa anakusudia kufungua ukurasa mpya wa kisiasa.

Matamshi haya aliyoyatoa wakati akiapishwa na baadaye akihutubia Bunge kwa mara ya kwanza, yalitoa mwanga wa matumaini.

Ni kwa kuzingatia hilo, Chama chetu kilichukua jukumu la kumwandikia Mh. Rais mwezi Mei 2021 kupendekeza masuala mbalimbali ya kufanyiwa kazi ili kufungua ukurasa Mpya wa kisiasa. Kwenye barua yetu kwa Mh. Rais iliyoandikwa na Kiongozi wa Chama chetu Ndugu Zitto Kabwe, tulipendekeza kwa Mh. Rais Katiba Mpya, Tume ya Uchaguzi, Mageuzi ya Jeshi la Polisi na kuandikwa upya kwa Sheria ya Vyama vya Siasa kuwa ni masuala makubwa ya kufanyiwa kazi ili kutekeleza adhma ya Mh. Rais ya kufungua ukurasa mpya wa kisiasa hapa nchini.

ACT Wazalendo tumeendelea na hoja hizi kwenye Kikao cha Wadau wa Tasnia ya Siasa kilichofanyika tarehe 15 hadi 17 Disemba jijini Dodoma.

Hata sasa, ACT Wazalendo tumeendelea kusimamia hoja hizo nne. Leo, Wanachama wa Dar es salaam mmepata heshima ya kuzindua rasmi Operesheni ya moja ya hoja hizo; Tume Huru ya Uchaguzi Kuelekea Katiba Mpya.

Ni Tume Huru ya Uchaguzi Kuelekea Katiba Mpya!

Ndugu Wanachama,
ACT Wazalendo tunaamini kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya havitenganishiki, vinategemeana. Kwa mazingira tuliyonayo, nchi yetu inahitaji Tume Huru ya Uchaguzi ili kupata Katiba Mpya yenye Maoni ya Wananchi Kama yalivyokusanywa, kuchambuliwa na kuwasilishwa na Tume ya Jaji Warioba.

Kwetu sisi ACT Wazalendo, Tume Huru ya Uchaguzi ni nyenzo ya kuhakikisha kuwa tunaipata Katiba Mpya itakayoweza kutumika nchini miaka mingi ijayo. Tume Huru ya Uchaguzi ni njia kuelekea kuipata Katiba Mpya.

Kwa muhtasari, tunahitaji Tume Huru ya Uchaguzi ili ifanye masuala yafuatayo;

1. Kuandaa na kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 ambao kwa muda uliobaki ni bayana kuwa utafanyika kabla hatujawa na hakika ya Katiba Mpya.

2. Kuandaa na kusimamia Uchaguzi Mkuu 2025 iwapo utafanyika kabla ya kupatikana kwa Katiba Mpya

3. Kusimamia kura ya Maoni ya Katiba Mpya ambayo ACT Wazalendo hatuafiki kusimamiwa na Tume ya Uchaguzi iliyopo.

Swali linalofuata bila shaka ni kwa namna gani Tume Huru ya Uchaguzi itapatikana? Ni kwa namna gani tutapata Tume Huru ya Uchaguzi kwa mazingira tuliyonayo?

ACT Wazalendo tunapendekeza kuandikwa upya kwa Sheria ya Uchaguzi na Kanuni zake ili kuunda Tume Huru ya Uchaguzi.

Kwenye Sheria hiyo, pamoja na mambo mengine, tunapendekeza kuundwa kwa Kamati ya Uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi. ACT Wazalendo tunapendekeza Kamati hiyo iwe huru na isimamiwe na watu wenye weledi, kuheshimika na kuaminika. Tunapendekeza Wajumbe wa Kamati hiyo watamkwe kisheria kuwa ni:

•Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Mwenyekiti,
•Jaji Mkuu wa Zanzibar kama Makamu wa Mwenyekiti,
•Rais wa Tanganyika Law Society awe Mjumbe,
•Rais wa Zanzibar Law Society awe Mjumbe,
•Mtu mmoja atakayeteuliwa na Mkuu wa Shughuli za Serikali Bungeni awe Mjumbe,
•Mtu mmoja atakayeteuliwa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni na kama hakuna Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni basi kutoka chombo kinachojumuisha Vyama vyenye Wabunge Bungeni awe Mjumbe,
•Mtu mmoja kutoka Asasi ya Kitaifa ya masuala ya Sheria na Haki za Binaadam Tanzania Bara awe Mjumbe,
•Mtu mmoja kutoka Asasi kama hiyo Tanzania Zanzibar awe Mjumbe,

Kwa vyovyote vile angalau theluthi ya wajumbe wa Kamati hiyo ya Uteuzi wawe Wanawake.


Bila shaka mnajiuliza vilevile, ACT Wazalendo tunataka Tume ya Uchaguzi iweje? Jibu letu ni bayana;

Hatutaki Tume ya Makada wa CCM, Tunataka Tume Huru!! Tunataka Tume itakayosimamia Uchaguzi kwa misingi ya haki, usawa na uhuru! Hatutaki Tume ya kusimamiwa na Watendaji wa Halmashauri ambao takribani wote ni Makada wa CCM!!

Tume ya Uchaguzi tunayoitaka ni ile ambayo Viongozi wake, Wajumbe na Watendaji wake watapatikana kwa mchakato wa wazi, huru na shindanishi.

Tunapendekeza kuunda Sheria mpya ya Uchaguzi (National Elections Act 2022) itakayoweka utaratibu kuwa Watanzania wanaotaka kuwa Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi waombe kazi kufuatia tangazo la wazi kwa umma.

Sheria hiyo ianzishe Kamati Maalum ya Uteuzi wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi kama nilivyowapambanua hapo awali.

Kisha, Kamati ya Uteuzi iliyoundwa kisheria, iwe na jukumu la kufanya usaili (interview) kwa uwazi kwa waombaji wote na kuchuja majina ambayo yatapelekwa kwa Rais kwa ajili ya uteuzi.

Baada ya kuteuliwa na Rais, Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume wataidhinishwa na Bunge kwa utaratibu utakaowekwa na Sheria ya Uchaguzi. Kisha watakula kiapo mbele ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano.

Mara baada ya wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi kupatikana watakuwa na jukumu la kuajiri Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye nafasi yake itatangazwa wazi kwa umma, kufanyiwa usaili wa wazi na kisha jina litakalopatikana kupelekwa kwa Rais kwa ajili ya uteuzi.

Tunahitaji kuwepo sifa maalum za Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi ili kuhakikisha wanakuwa watu wenye weledi na hawaegemei upande wowote.

Wasimamizi wa Uchaguzi na Watendaji wa Tume kutoka ngazi ya Taifa, Majimbo, Kata hadi ngazi za chini wawe waajiriwa wa Tume kwa utaratibu wa wazi na kwa kuzingatia sifa na vigezo vya uwezo na weledi. Mtindo wa makada wa Chama tawala kugeuzwa kuwa Wasimamizi na Watendaji wa Tume, tunataka ukomeshwe na uungwaji wa Tume Huru mpya tunayoikusudia.

Ndugu Wanachama, katika kuhitimisha, naomba nisisitize kuwa kipindi cha kuelekea kupatikana kwa Katiba Mpya ni cha kipekee. ACT Wazalendo tunao wajibu wa kuonesha uongozi katika kipindi hiki. Kwa maoni yetu, katika kipindi hiki mambo kadhaa yanapaswa kufanyika kama ifuatavyo;-

1. Marekebisho makubwa au kuandikwa upya kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sheria ya Kura ya Maoni;

2. Kuandikwa upya kwa Sheria ya Uchaguzi na Kanuni zake na Kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi; na

3. Muafaka wa Kitaifa ili kupata Katiba Bora.


Ndugu Wanachama,
Ili kufikia hatua hizo, ni lazima kuwe na maridhiano ya dhati miongoni wa viongozi wa kisiasa na wadau wa kisiasa kwa ujumla wake. Chama chetu kinafahamu ujenzi wa maridhiano unataka kuwa tayari kukaa mezani, kuzungumza na kuelezana ukweli kwa ajili ya kufungua ukurasa mpya. Chama chetu kitaendelea kushirikiana na Vyama vingine vya Siasa na wadau wa Demokrasia kujenga Maridhiano ya dhati.

Ndugu zangu, hoja yetu ya Tume Huru ya Uchaguzi Kuelekea Katiba Mpya yenye Maoni ya Wananchi ndio hoja sahihi kwa mazingira tuliyonayo. Baada ya kuizindua rasmi hapa leo, tutaipeleka kila kona nchini. Ni wajibu wa kila Mwanachama kuielewa kwa kina na kuisambaza kwa umma. Ninawatakia kila la heri viongozi wote katika kuutekeleza wajibu huu.

TUME HURU na KATIBA MPYA ni sasa!!


Juma Duni Haji,
Mwenyekiti wa Chama Taifa,
ACT Wazalendo.
20 Machi 2022.
Dar es salaam.

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK