Wanachama kuamua hatma ya SUK, Kamati Maalum ya Kamati Kuu Zanzibar yaelekeza.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Kamati Maalum ya Kamati Kuu ya Chama cha ACT WAZALENDO upande wa Zanzibar imekutana leo tarehe 15 Novemba, 2022 katika Ofisi Kuu ya Makao Makuu ya Chama, Vuga, Zanzibar chini ya Uenyekiti wa Makamo Mwenyekiti wa ACT Wazalendo (Zanzibar) Ndugu Othman Masoud Othman.

Kikao hicho cha dharura kimeitishwa kujadili hali ya kisiasa Zanzibar kutokana na taharuki ya kisiasa iliyoibuka kufuatia uteuzi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ZEC Ndugu Thabit Idarous Faina ambaye ndiye aliyesimamia Uchaguzi Mkuu wa 2020 uliosababisha mauaji na maafa makubwa katika nchi. Uteuzi huo ukiambatana na matukio mengine yasiyoridhisha katika kipindi cha miaka miwili iliopita umesababisha Wazanzibari kupoteza imani na kutilia shaka uwepo wa dhamira njema na nia ya dhati ya kujenga maridhiano ya kweli na umoja wa kitaifa kama ilivyokuwa imeahidiwa.

Kamati Maalum ya Kamati Kuu ya Chama upande wa Zanzibar baada ya kupokea taarifa iliyowasilishwa imeielekeza Sekretarieti ya Chama upande wa Zanzibar kuratibu vikao vya ndani vya viongozi, wanachama na wafuasi wa Chama kusikiliza na kutoa maelekezo yao juu ya mustakabali wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na hali ya kisiasa Zanzibar.

Kamati Maalum imesisitiza kwamba vikao hivyo vya ndani vya kusikiliza maoni ni utekelezaji wa ahadi ya uongozi wa Chama Taifa ya kusikiliza maoni na tathmini ya Wanachama baada ya Miaka miwili ya ujenzi wa Maridhiano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kamati Maalum imeagiza ripoti ya vikao hivyo iwasilishwe kwenye Kikao cha Kamati Kuu ya Chama.

Imetolewa na:

Salim A. Bimani,
Katibu wa Habari, Uenezi, Mawasiliano na Umma,
ACT-Wazalendo
15/11/2022

Showing 1 reaction

Please check your e-mail for a link to activate your account.

Ukurusa huu unatumia kuki. Kusoma zaidi, angalia Vigezo na Masharti yetuOK